Kutoka kwa Msajili wa Hazina
Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar ilianzishwa kwa Sheria Namba 6 ya 2021, baada ya kufutwa kwa Sheria Namba 4 ya 2002. Lengo lake ni kusimamia mali za umma na uwekezaji kwa ufanisi kupitia sera, sheria, na miongozo, ili kuhakikisha taasisi za uwekezaji wa umma zinafanya kazi kwa viwango bora na zenye tija.
Utangulizi
Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imeanzishwa kwa Sheria Nambari. 6 ya mwaka 2021, Sheria ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Usimamizi wa Mali za Umma. Sheria hii inatokana na kufutwa kwa Sheria Nambari 4 ya mwaka 2002 Sheria ya Mitaji ya Umma.
Dira ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ni Kuwa chombo chenye ufanisi cha uwekezaji wenye tija na usimamizi wa mali za umma na dhamira ya Kuweka Sera, Sheria, Miongozo na vigezo vya usimamizi ili kuhakikisha Taasisi za uwekezaji wa Umma zinakuwa zenyekuleta tija katika viwango bora.
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 shughuli za usimamizi, uhakiki wa Mali za Serikali na Mitaji ya Umma kwa nyakati tofauti zimekuwa zikisimamiwa na Idara mbali mbali ikiwemo Idara ya Hazina, Idara ya Uhakiki Mali na Idara ya Mitaji ya Umma. Kuanzia mwaka 2005 Idara ya Uhakiki Mali na Idara ya Mitaji ya Umma ziliunganishwa na kuwa Idara ya Uhakiki Mali na Mitaji ya Umma, lengo kuu la kuziunganisha idara hizi ni kuleta ufanisi zaidi katika kazi za usimamizi wa Mali za Serikali na Mitaji ya Umma.
Katika kuendeleza udhibiti wa Mali za Serikali Ofisi ya Rais fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo iliendelea kuandaa mikakati mbalimbali ya kusimamia Mali za Serikali kwa kuanzisha Sheria ya Mitaji ya Umma No 4. ya mwaka 2002 ambayo hadi sasa imeweza kusimamia Mitaji ya Umma, hisa za Serikali na Mashirika ya Umma ili yaweze kujiendesha kibiashara na kwa faida, kuleta maendeleo na hatimae kuweza kuchangia mapato ya Serikali na kukuza Uchumi wa taifa.